TUCTA KUITISHA MGOMO NCHI NZIMA
SHIRIKISHO la Vyama Vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), linatarajia kuitisha mgomo wa wafanyakazi nchi nzima, endapo Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) haitaondoa kanuni mpya ambayo inaruhusu watumishi watakaostaafu kwa hiari yao kukatwa asilimia 18 ya mafao yao.
Kanuni hiyo mpya itaanza kutumika Julai mwaka huu ambapo watumishi watakaostaafu kwa hiari watalazimika kukatwa kiasi hicho.
Ili kuhakikisha suala hilo linashughulikiwa ndani ya muda mwafaka, TUCTA imeazimia kuitisha mkutano mkuu unaotarajiwa kufanyika Aprili 23 na 24, mwaka huu ili kujadili suala hilo.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na MTANZANIA mjini Dar es Salaam jana, Rais wa shirikisho hilo, Gratian Mukoba alisema kanuni hiyo ni kandamizi na inawanyima haki watumishi kwa sababu kulipwa mafao ni haki ya mtumishi aliyestaafu, ingawa pia wakati wanajadili kuipitisha hawakushirikishwa.
“Tutawahamasisha watumishi kugoma nchi nzima ili kuishinikiza SSRA kubadili kanuni hii kwa sababu ni kandamizi kwa mtumishi.
“Bila ya kufanya hivi, Serikali itaendelea kutunga kanuni nyingine ambazo zinaweza kutoa nafasi kwa watumishi kuendelea kufanya kazi hadi miaka 70 ili wakifariki kabla ya muda huo wawe wamepoteza mafao yao, kutokana na hali hii, hatutakubali na tunataka iondolewe mara moja,”alisema Mukoba.
Alisema kutokana na hali hiyo, shirikisho hilo linasubiri majibu ya barua hiyo na endapo hawasikilizwa watafanya mgomo huo.
“Baada ya kuona kanuni hii haifai, tumewaandikia barua SSRA ili waweze kutupa ufafanuzi,ikiwa hawajatupa majibu tutawahamasisha watumishi nchi nzima kugoma kama walivyofanya madereva,”alisema.
Alisema wakati SSRA inapitisha kanuni hiyo, tayari Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliiagiza mamlaka hiyo kurudi meza ya mazungumzo na wadau ili waweze kujadili kanuni tata inayoelekeza SSRA kutoa asilimia 25 badala ya asilimia 50 ya mafao yao.
“Bado tupo kwenye mgogoro na SSRA kuhusiana na kanuni tata ambayo inatumika sasa ya kutulipa asilimia 25 badala ya asilimia 50 ya mafao yetu,”alisema.
Alisema tangu agizo hilo litolewe hakuna utekelezaji wowote badala yake wameamua kutunga kanuni nyingine ambayo ni kandamizi zaidi.
Afisa Uhusiano wa SSRA, Sarah Kibonde alipoulizwa juu ya madai hayo, alisema kanuni mpya ya ukokotoaji haijaweka kiwango hicho cha makato na kanuni inahusu wafanyakazi walioajiriwa kuanzia Julai mwaka jana.
CHANZO: Mtanzania(15/04/2015)
Post a Comment